Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Republican, Donald Trump anazidi kuwekwa kwenye wakati mgumu wa kushinda uchaguzi wa mwezi Novemba baada ya wataalamu wa masuala ya usalama wa chama hicho kusaini barua ya kutomuunga mkono mgombea huyo.
Wataalamu hao 50 wamesaini baruaya wazi ambayo inaonya kuwa endapo Trum atapewa uongozi wa nchi hiyo, Marekani kwa mara ya kwanza itakuwa imepata rais ‘mbumbumbu zaidi’ katika historia yake.
Kundi hilo la wataalamu wa usalama ambalo linamjumuisha mkurugenzi wa zamani wa shirika la kijasusi la Marekani, CIA Michael Hayden, limesema kuwa Bw. Trump ‘hana hadhi, maadili na uzoefu’ wa kuwa rais.
Hata hivyo wajumbe wengi waliosaini barua hiyo hivi sasa ndio wajumbe waliokataa kusaini barua hiyo mwezi Machi mwaka huu hiyo ikiashiria kuwa kwenye kipindi cha miezi mitano wamefanya tathmini na kuja na msimamo tofauti.
Bw. Trump kwenye msimamo wake dhidi ya watu hao amedai kuwa, watu hao ni sehemu ya ‘mamlaka iliyoshindwa’ na wanafanya hivyo ili wabaki madarakani.
Barua hiyo ya wazi imekuja kufuatia kundi kubwa la wanachama wa Republican wenye nafasi za juu kukataa kumuunga mkono mfanyabiashara huyo mkubwa.
‘[Trump] Anadhoofisha mamlaka ya kimaadili ya Marekani akiwa kama rais wa dunia huru. Anaonekana kukosa ufahamu wa msingi kuhusu imani ndani ya katiba ya Marekani, sheria za Marekani na taasisi za Marekani ikiwemo uvumilivu wa imani za kidini, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa mahakama’ inasema sehemu ya barua hiyo.
‘Hakuna yeyote miongoni mwetu atakayempigia kura’ imeongeza barua hiyo Kwenye taarifa yake, Trump amesema kuwa majina ya watu waliosaini barua hiyo ni watu ambao wamarekani wanapaswa kuwahoji ‘kwanini dunia imechafuka’,.