Wasanii wa muziki wanaoweka kazi zao kwenye akaunti zao binafsi za mtandao wa Youtube hawatalazimika kusajiliwa na Mamlakaya Mawasiliano Tanzania (TCRA) au kulipia ada kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara hiyo pamoja na TCRA, wameshakubaliana kubadilisha Kanuni hiyo kwa wasanii na wadau wengine wa maudhui yasiyohusisha uchakataji wa habari.
Akizungumza na Viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na vyama vinavyounda shirikisho hilo Jijini Dar es Salaam Aprili 20 2021, Dkt. Abbasi amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kuona umuhimu wa kuwanufaisha Wasanii na kukuza Sanaa nchini.
Mabadiliko hayo yatalenga kuwaweze wasanii na wadau wengine wa maudhui yasiyohusisha uchakataji wa habari kurusha kazi zao kwenye akaunti zao binafsi za YouTube bila kufanya usajili na malipo kwa TCRA.
“Tumefanya mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na TCRA kuhusu maudhui ya TV za mtandaoni, tumeona kuna tofauti kubwa sana kati ya Habari na Sanaa, hivyo tutaboresha kanuni…” amesema Dkt Abbasi
Tumeona eneo hili la Wasanii linapaswa kufanya kazi zao bure, sasa nafurahi kuwaambia kuwa kuanzia sasa wasanii wawe wa muziki au filamu changamoto hii imefika mwisho,” aliongeza.