Wanyama jamii ya twiga wamepungua sana duniani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na kwa sasa wanakabiliwa na hatari ya kuangamia kabisa katika ulimwengu.
Idadi ya twiga duniani imeshuka kutoka 155,000 mwaka 1985 hadi 97,000 mwaka 2015 kwa mujibu wa shirika la kimataifa la uhifadhi wa mambo asilia (IUCN).
Idadi ya wanyama hao imepungua sana kutokana na kuharibiwa kwa maeneo wanamoishi, uwindaji haramu na migogoro ya kisiasa katika maeneo mengi Afrika.
Baadhi ya aina wa twiga, sana maeneo ya kusini ya Afrika, wanaongezeka hata hivyo.
Hadi kufikia sasa, IUCN hawakuwa wameorodhesha twiga kuwa miongoni mwa wanyama walio hatarini.
Hata hivyo, kwenye orodha yao mpya ya wanyama walio hatarini, mnyama huyo ameorodheshwa kuwa “hatarini”, baada ya idadi ya wanyama hao kushuka kwa zaidi ya asilimia 30.
Ongezeko kubwa la idadi ya watu limesababisha maeneo mengi ya misitu kuharibiwa kwa ajili ya kilimo, jambo ambalo limepunguza maeneo wanamoishi twiga.
Vita katika baadhi ya maeneo Afrika pia vimeathiri idadi ya wanyama hao.