Wanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamesema wamemshauri Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe asiende kuripoti polisi leo.
Mwanasheria wa Chadema, John Mallya amesema Mbowe hatakwenda kuripoti polisi leo kwa sababu amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam na inaanza kusikilizwa Februari 21 mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema yuko Mwanza na hajawasiliana na Mbowe.
Alipoulizwa kama Mbowe atakamatwa wakati wowote kuanzia sasa, Lissu alisema watalazimika kulishtaki mahakamani Jeshi la Polisi kwa kitendo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina 65 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo Mbowe.
Pamoja na kutaja majina hayo, Makonda aliwaagiza watuhumiwa hao kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma hizo.
Februari 10 mwaka huu, akiwa mjini Dodoma, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alizungumza na waandishi wa habari na kusema hajawahi kujihusisha kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya na pia hatakwenda polisi kuhojiwa kama alivyoagizwa na Makonda.