Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabara nchini kimefanya msako maalum wa kuyakamata mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze na Msata ambao hukatisha ruti.

Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Pwani Abdul Isango amesema polisi imeendesha zoezi hilo kufuatia malalamiko ya abiria wengi kufika kituo cha polisi kulalamikia tabia ya madereve kuishia njiani na kutumia lugha za matusi pindi wanapodai haki yao.

Kamanda Isango amesema malalamiko hayo mara nyingi yametokea kwa mabasi aina ya Costa ambayo yanafanya safari zake kwenda Msata, Mkata, Chalinze hadi Mlandizi ambao mara nyingi huishi maeneo ya Kongowe, Kibaha mkoani Pwani.

Kamanda huyo amesema matukio hayo ni endelevu na watafanya utaratibu huo maalum kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuwavisha askari mavazi ya kiraia ili kuwabaini madereva wanaoendeleza makosa hayo ambayo yanakiuka leseni zao walizopewa za usafirishaji wa abiria.

Pia kamanda Isango amesema katika msako huo jumla ya magari kumi yamekamatwa na madereva wake wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za SUMATRA nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *