Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu uwepo wa Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos), inayotapeli watu fedha kwa kutumia majina ya watu maarufu nchini.
Tahadhari hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema Saccos hiyo yenye jina maarufu la Focus Vicoba kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na tovuti inayojulikana kwa jina “http://www.vicobaloanstz. wapka-mob” www.vicobaloanstz. wapka-mob, hutumia majina ya viongozi serikalini na watu maarufu, kwa nia ya kuwatapeli wananchi.
Pia amesema majina ya viongozi yanayotumiwa na matapeli hao ni pamoja na jina la mke wa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Ameongeza kuwa matapeli hao, hutumika kufungua akaunti za facebook na tovuti mbalimbali, ambazo hutumia kuwarubuni watu kwa kuwaaminisha kuwa wanaweza kupata mikopo yenye masharti nafuu na haraka zaidi kwa njia hiyo ya mtandao.