Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia, Profesa Joyce Ndarichako amesema kuwa wanafunzi wa St. Joseph walioamishiwa katika chuo kikuu cha Dodoma kurudia mwaka kwa kile kilichobainika kuwa na ujuzi na maarifa usiokidhi viwango vya chuo cha Dodoma.
Wizara hiyo pia imesema kwamba watakaogomea uamuzi huo watatakiwa kurudi makwao.
Profesa Ndarichako amesema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU.
Prof. Joyce Ndalichako amesema ni lazima wanafunzi hao warudie mwaka kwani wamepimwa na kubainika kuwa na uwezo mdogo hivyo hatua ya kuwataka kurudia mwaka ni nafasi ya pili kwao.
Pia amesema kwa sasa wizara yake inaandaa ripoti ya vyuo vinavyofundisha chini ya viwango ambapo amesema mara tu baada ya kukamilika ripoti hiyo, itatolewa na kwamba kwa wale wanafunzi ambao vyuo vyao vimefungwa kwa kutokidhi vigezo ni lazima wapimwe kiubora ili kupata wanafunzi watakao kidhi vigezo vya soko la ajira.
Vile vile Ndalichako ametoa onyo kwa wanafunzi ambao wamegushi nyaraka mbalimbali ikiwemo za vifo vya wazazi wao ama ugonjwa na kufanikiwa kupata mkopo wa elimu ya juu kwa njia ya udanganyifu kuwa wizara hiyo inafanya uhakiki na pindi watakapo bainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.