Watoto watatu wa shule ya msingi ya Lucky Vicent walionusurika katika ajali ya basi, wamefanyiwa upasuaji nchini Marekani.
Baada ya upasuaji huo kwasasa wanaendelea vizuri na wapo wodini wakiendelea na mazoeazi.
Taarifa hiyo imetolewa na mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) Lazaro Nyarandu kupitia ukurasa wake wa facebook ambapo amesema watoto hao kwa sasa wamewekwa kwenye vyumba vya peke yao.
Upasuaji huo umefanyika katika Hospitali ya Mercy, Sioux City, Marekani ambapo watoto hao wamepelekwa kwa matibabu.
Amefafanua upasuaji waliofanyiwa na kusema mtoto Saidia alifanyiwa upasuaji wa mfupa wa kulia wa nyonga, mkono wa kulia na kuwekewa ngao kwenye shingo atakayotakiwa kukaa nayo kwa wiki sita.
“Kwa upande wa mtoto Wilson, yeye amefanyiwa upasuaji wa nyonga ya kulia, kiwiko cha kulia kilichokuwa kimevunjika mara tatu na kiwiko cha kushoto,” amesema
Amesema Doreen yeye amefanyiwa upasuaji wa nyonga, taya katika upasuaji uliochukua saa nne na leo atafanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo.