Wafanyakazi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Mji wa Dodoma (CDA) wamepangiwa vituo vipya vya kazi.
Kwa mujibu wa Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wafanyakazi 150 kutoka kundi hilo wanabaki Manispaa ya Dodoma huku wengine 66 wakipelekwa katika halmashuri na mikoa mbalimbali nchini.
Amesema wafanyakazi 16 wamepelekwa Tamisemi, DART (14), Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma (4), Chuo Kikuu cha Dodoma (3), Ofisi ya Waziri Mkuu (3), Wizara ya Ardhi (2) Ofisi ya Bunge (1) na Utumishi wa Umma (1).
Waziri Simbachawene amewataka wafanyakazi hao kuripoti katika vituo vyao vya kazi mara baada ya kupata barua na Serikali haitasita kufuta ajira ya mtumishi yeyote ambaye atakaidi agizo hilo.
Rais wa John Magufuli aliivunja rasmi CDA Mei mwaka huu na kuagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Rais Magufuli alisema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
CDA ilianzishwa kwa Amri ya Rais ya Aprili Mosi, 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230.