Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kuwakamata na kuwafikisha mahakamani viongozi wote wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) na wa taasisi za kibenki, ambao wamewaibia wakulima wa korosho Sh bilioni 1.7 hadi watakapozirejeresha.
Ameyasema hayo jana wilayani Masasi mkoani Mtwara, wakati alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika Uwanja wa Sabasaba.
Waziri Mkuu amesema serikali imejitahidi kuboresha bei ya zao la korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Lakini, alisema watu wachache wanataka kutia dosari jitihada hizo, kwa kutaka kumnyonya mkulima na kujinufaisha kwa masilahi yao binafsi, jambo lilonarudisha nyuma jitahada za wakulima katika kujiletea maendeleo kupitia zao la korosho.
Amesema, watendaji wa taasisi za kibenki hususani Benki ya NMB, wametajwa kuwa ni miongoni mwa watu wenye tabia ya kushirikiana na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi katika kuwaibia wakulima fedha zao za korosho, jambo ambalo linasababisha kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima kudai fedha zao kuwa hajalipwa licha ya kuuza korosho kwenye minada.
Waziri Mkuu amesema serikali haitakaa kimya na kuona baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi na wale wa Benki ya NMB, wakiendelea kuwaibia wakulima fedha zao, bila ya kuwachukulia hatua.
Alisema kuanzia sasa lengo ni kuwatokomeza wanyonyaji wote kwenye zao la korosho, ambao huwaibia wakulima.
Alisema serikali itaendelea kuwakamata viongozi wote wa vyama vya msingi, ambao ni wezi kwenye zao la korosho na itahakikisha inawafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.