Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu ambao ni wanafunzi walioshiriki kitendo cha kumpiga mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya kutwa ya Sekondari ya Mbeya.
Walimu hao ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi huyo kwa makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa Duce na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Aidha, serikali imemvua madaraka Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kwa kutochukua hatua baada ya kitendo hicho kufanyika shuleni hapo Septemba 28, mwaka huu.
Profesa Ndalichako amesema kitendo hicho ni cha kikatili, jinai na kuwa walimu hao wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Profesa Ndalichako ameongeza kwa kusema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo kilichofanywa na walimu wanafunzi hao ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi kufumbiwa macho.
Pia ametoa onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na kwenda kinyume cha taaluma yao kuwa wanapoteza sifa hivyo amewataka kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazosomea.
Kwa upande mwingine Kamanda wa Polisi wa Mkoani Mbeya, Dhahiri Kidavashari amesema wanawashikilia walimu wa shule hiyo watano kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.
Kama Kidavashari amesema si kwamba walimu hao wanaohojiwa ndio waliohusika na tukio hilo bali wameanza na wale waliopo ili kupata taarifa zaidi.