Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo la kutaka madai sugu ya walimu katika Jiji la Arusha yalipwe ndani ya siku 14 limezaa matunda, kwani madai yao yote yaliyofikia zaidi ya Sh milioni 169.7, yamelipwa.
Gambo ametoa agizo hilo alipokutana na walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani Arusha waliompa malalamiko mengi, likiwemo la madai sugu ya walimu na hapo hapo Mkuu huyo aliagiza halmashauri zote na Jiji mkoani humo kulipa madeni hayo ndani ya siku 14.
Katika kutekeleza agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro alisema Jiji limetekeleza ndani ya siku mbili na kufanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kwa walimu wote wa msingi na sekondari.
Daqarro amesema Jiji la Arusha lina jumla ya walimu 701 wa msingi na sekondari na madai yao yote yamelipwa ndani ya muda huo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inawajali na kuwalinda walimu wote na kuwapa stahili zao za msingi kwa wakati bila ya kipingamizi chochote.
Mkuu huyo alisema walimu walikuwa wakidai stahili zao za muda mrefu, ikiwa ni pamoja na fedha za kujikimu, likizo, nauli, matibabu na upandishwaji madaraka na fedha hizo zote wamelipwa.
Amesema kwa sasa serikali ya wilaya ya Arusha inataka kuona walimu wakifanya majukumu yao ya msingi katika kupandisha elimu ikiwa ni pamoja na kufundisha wanafunzi bila ya kuwa na mawazo.
Akizungumzia upatikanaji wa fedha hizo kwa muda huo mfupi alisema Halmashauri ya Jiji la Arusha iliamua kusitisha malipo yasiyokuwa ya lazima au kuondoa malipo ambayo yako kinyume na taratibu na ndiyo maana fedha hizo zimepatikana.
Mkuu huyo alisema si kwamba fedha za kuwalipa walimu zilikuwa hazipo, bali zilikuwa zikilipa vitu vilivyo nje ya utaratibu na kutokana na usimamizi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia ameweza kubana mianya yote ya ulaji fedha.