Kampuni ya kuchimba madini ya Acacia Mining Plc, imesema Mwenyekiti wa Barrick, Profesa John Thornton ambaye alifanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli, Ikulu Dar es Salaam juzi, hakusema kama watalipa malimbikizo ya kodi.
Acacia ilitoa ufafanuzi huo jana katika mkutano wa wanahisa baada ya mwanahisa mmoja kutaka kujua kama ni kweli kampuni hiyo ilitoa ahadi ya kulipa malimbikizo ya kodi za nyuma ambazo haikulipa kwa Serikali ya Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, aliwaambia wanahisa kupitia mkutano kwa njia ya simu kutokea makao makuu ya kampuni hiyo London, Uingereza jana kuwa mwenyekiti huyo hakuzungumza chochote kuhusu kulipa kodi.
Akiwa na mkuu wa kitengo cha fedha wa kampuni hiyo, Andrew Wray, Gordon alisema ripoti ya kamati ya pili iliyotolewa Jumatatu Juni 13, mwaka huu haikuwa nzuri kwa Acacia, lakini haikuwashangaza kwa kuwa walitegemea ingekuwa hivyo.
Wakati Acacia wakisema hivyo, taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu na video ya Rais Magufuli ilieleza kwamba katika mazungumzo yao wamekubaliana kuunda timu mbili za majadiliano.
Alisema timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick kutoka Canada na Marekani na watafanya majadiliano ambayo yatahusu namna ya kufikia mwafaka kwenye suala la kusafirisha mchanga wa madini (makinikia) nje ya nchi kwa faida ya pande zote mbili.
Kupitia taarifa hiyo, Rais Magufuli alisema timu hiyo itapitia mapendekezo yote na Profesa Thornton amekubali chochote ambacho kitakuwa kimekubalika watalipa.