Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwele amesema serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza mradi wa kutoa maji katika mto Ruvuma kwenda katika manispaa ya Mtwara ili kuwanufaisha wakazi wanaosumbuka na huduma ya maji kwasasa.
Dkt. Kamwele ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini kupitia tiketi ya (CUF) Maftah Nachuma aliyetaka kujua kuhusu hatma ya mradi huo, huku akiituhumu serikali kukwamisha mradi huo kwa kuzuia kibali.
Naibu Waziri Kamwele amesema siyo kweli kwamba serikali inakwambisha mradi huo kwa kuzuia kibali bali mazungumzo kati ya serikali na benki ya Exim yamekamilika na wamekubali kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo.
Aidha Naibu Waziri huyo amesema kwamba serikali inatambua kero ya maji kwa wakazi wa Bagamoyo na imeshamuagiza mhandisi mshauri kuangalia namna ambavyo bomba linalotoa maji mto Ruvu kuja Dar es Salaam linaweza kugawanyishwa katika maeneo mbalimbali ili wananchi waweze kupata maji ambapo Mji wa Bagamoyo utanufaika na mpango huo.