Wafugaji watano wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wamejeruhiwa kwa risasi huku mmoja amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete baada ya kuvamia hifadhi ya wanyamapori.
Wafugaji hao wanadaiwa kuvamia kambi ya hifadhi ya wanyamapori iliyopo Kijiji cha Utimule Kata ya Ngoywa na kutaka kuchukua mifugo yao iliyokamatwa.
Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori kutoka Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Magharibi, Nasser Alli amesema wafugaji zaidi ya 40 walijikusanya na kuvamia kambi kwa lengo la kuchukua mifugo yao.
Amesema usiku mmoja kabla ya tukio alipokea simu ya mtumishi mwenzake akimjulisha amepigiwa simu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Peter Nzalalila, kuwa kuna wafugaji wanataka kuvamia kambi hiyo ili kuchukua ng’ombe wao 200.
Amesema wafugaji waliweza kuvamia kambi hiyo na kuanza kuwashambulia kwa silaha za jadi kama sime, mikuki, upinde na fimbo lakini askari walipambana na kufanikiwa kuwakamata wafugaji watano huku wengine wakitoroka.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Kitete, Dk. Benedicto Komba amesema alipokea majeruhi hao huku mmoja akiwa amevunjika miguu miwili kwa kupigwa risasi.