Wafuasi wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad walipigana hadharani katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Ugomvi huo ulioibua mapambano ya ngumi ulitokea jana baada ya wafuasi wa Maalim Seif waliokuwa mahakamani hapo kumzuia Profesa Lipumba kuingia kusikiliza kesi inayomkabili iliyofunguliwa na Baraza la Wadhamini wa Chama hicho.
Profesa Lipumba alifika mahakamani hapo saa mbili asubuhi, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kesi hiyo dhidi yake kufunguliwa ikidai kuwa yeye si mwanachama halali wa CUF.
Baada ya kesi za Jaji Sakiet Kihio kuitwa na mtoa matangazo wa Mahakama kwa kuelekeza kuwa kesi za Jaji huyo zinasikilizwa chemba watu wote waliinuka na kuelekea katika chumba hicho wakiwamo mawakili wa pande zote.
Walipofika kwenye mlango wa chumba cha Mahakama, wafuasi wa Maalim Seif walisimama mlangoni kumzuia Profesa Lipumba kwa madai kuwa wanaotakiwa ni mawakili tu na si watu wengine, ndipo wafuasi wa Mwenyekiti huyo walipoingilia kati na kuwashushia kipigo watu hao.
Hatua hiyo ilishuhudia mabadilishno ya makonde na kusababisha watu wawili upande wa Maalim Seif kuumia, na kusababisha Jaji Kihio kutoa amri kuwa waingie mawakili na walalamikiwa ndipo Lipumba naye akaingia.
Kesi iliendelea kusikilizwa, huku askari wakiimarisha ulinzi wa chumba hicho, kwa sababu wakati wafuasi hao wanapigana wao hawakuwapo. Jaji Kihio aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6 zitakaposikilizwa sababu za Bodi hiyo kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Profesa Lipumba alitolewa na wafuasi wake akiwa chini ya ulinzi mkali kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayemgusa na alipofika nje, alipokewa na wafuasi wengine wakiwa na mabango yenye ujumbe dhidi ya Maalim Seif.