Wafuasi wa rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wameandamana nje ya mahakama kuu mjini Nairobi wakiwashutumu majaji wa mahakama kuu kwa kuwaibia ushindi wao.

Majaji wa mahakama hiyo walitoa uamuzi wa kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 8 Agosti yaliyompatia ushindi Kenyatta baada ya kusema kuwa mchakato wake ulikuwa si huru na haki.

Maandamano hayo yamefanyika wakati gazeti la The Standard kuchapisha taarifa ya madai kwamba majaji wawili wa Mahakama kuu , Philemona Mwilu na Isaac Lenaola, ambao walipigia kura kubatilishwa kwa uchaguzi, walikutana na mawakili wa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Taarifa hiyo iliyotawala mazungumzo ya raia wa Kenya kwenye mtandao wa Twitter,pia inasema kuwa kuna mazungumzo ya simu yaliyo rekodiwa kuthibitisha kwamba kulikuwa na mawasiliano baina ya majaji na mawakili wa upinzani waketi kesi hiyo ikiendelea.

Waandamanaji hao wamekwisha wasilisha madai yao kwa tume ya huduma za mahakama inayowaajiri na kuchunguza mienendo ya majaji nchini Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *