Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii imetoa muda wa wiki moja kwa wadau wa habari kuhakikisha wanawasilisha maoni yao kwa ajili ya kuboresha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.

Kabla ya agizo hilo, wadau hao wa habari, waligoma kutoa maoni yao katika kikao hicho cha kupokea maoni ya wadau, wakiomba kuongezewa muda wa takribani miezi minne ili waweze kushirikisha wadau wengi zaidi kuupitia muswada huo na kutoa maoni yao kwa mrengo mmoja.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Serukamba, amesema Bunge haliwezi kuahirisha shughuli zake kwa sababu ya kusubiria maoni ya wadau.

Awali, katika kikao hicho kilichotarajiwa kupokea maoni hayo ya wadau, uliibuka mjadala mzito uliotawaliwa na mabishano miongoni mwa wabunge wenyewe na wadau hao kuhusu suala la kushirikishwa kwa wadau wa habari katika mchakato mzima wa kuandaa muswada huo.

Akiwasilisha kwa niaba ya MOAT Katibu Mtendaji wa chama hicho, Henry Mwanika, alisema chama hicho bado kinaendelea kukusanya maoni kwa wadau wake mbalimbali wakiwemo wa mikoani kwani muda waliopatiwa kwa ajili ya kuupitia muswada huo hautoshi.

Naye Mwakilishi wa MCT, Pili Mtambalike, alisema pamoja na kwamba mchakato wa kuanzishwa kwa sheria hiyo ya habari una takribani miaka 10 sasa, muswada uliosomwa hivi karibuni bungeni umebainika kuwepo na baadhi ya vifungu vinavyohitaji umakini.

Alitaja baadhi ya vifungu hivyo kuwa ni pamoja na kifungu kinachompa mamlaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kungóa mitambo ya uchapishaji katika chombo chochote cha habari endapo atahisi au kubaini kuwa kinachapisha taarifa yeyoye yenye kashfa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *