Wabunge nchini Marekani wamemtaka Rais wa nchi hiyo Donald Trump kusalimishe kanda ya mazungumzo yoyote yaliorekodiwa kati yake na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la FBI, James Comey.

Kiongozi wa Chama cha Democrats katika Bunge la Seneti, Charles Schumer alionya kuwa uharibifu wa kanda hizo utakuwa uvunjaji wa sheria.

Naye Seneta wa Republican, Lindset Graham amesema kuwa Ikulu ya Whitehouse inahitaji kuwa wazi kuhusu iwapo kulikuwa na kanda zozote za rekodi za mazungumzo hayo au la.

Matamshi hayo yanajiri baada ya Rais Trump kuandika katika akaunti yake ya Twitter matamshi yanayoonekana kuwa vitisho kwa mkuu huyo wa zamani wa FBI.

Alimuonya Comey wiki iliopita dhidi ya kuzungumza na vyombo vya habari akisema natumai hakuna rekodi za mazungumzo yetu.

Ikulu ya Whitehouse haijathibitisha wala kukana kuwepo kwa kanda hizo za mazungumzo kati ya Trump na Comey.

Bwana Schumer pia alionya kwamba masenata wa chama cha Democrats watakataa kumuunga mkurugenzi mpya wa FBI hadi pale mtaalam atakapochaguliwa kuchunguza hatua ya Urusi kuingilia maswala ya Marekani katika uchaguzi uliopita.

 

FBI inachunguza madai hayo pamoja na ushirikiano wa Urusi na kampeni ya rais Trump ambapo hata hivyo rais huyo amekana uhusiano wowote na anasema bwana Comey amemhakikishia kwamba hachunguzwi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *