Wabunge wa Uganda waliokuwa safarini kikazi nchini Afrika Kusini wamelalamika kuvamiwa na vibaka na kuporwa mali zao ikiwemo hati za kusafiria.
Wabunge waliokumbwa na mkasa huo ni Robert Ndugwa Migadde, Santa Sandra Alum, Francis Barnabas Gonahasa, Kenneth Esiangu Eitunganane, Florence Aceng, Jacquiline Mutekanga, Dr Moses Achong Ongom na Christine-Doreen Lowila Oketayot
Tayari mamlaka za Afrika Kusini na Uganda zimeanza uchunguzi wa tukio hilo ambalo huenda likapelekea kutetereka kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo.
Gazeti la Uganda la Monitor limedai kuwa tukio hilo lilitokea kwenye maeneo mbalimbali na kwa nyakati tofauti ambapo baadhi ya wabunge hao waliporwa wakiwa kwenye kizuizi cha ukaguzi wa askari.
Wabunge hao walikuwa kwenye ziara ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza mbolea nchini humo.
Kwenye tukio hilo inadaiwa kuwa mmoja wa wabunge hao alivuliwa nguo kwenye nyumba ya kulala wageni ya KariBou-Inn Guest House iliyopo kwenye jiji la Johannesburg.
Wabunge waliovamiwa na kuporwa kwenye sehemu ya ukaguzi ni Robert Ndugwa Migadde, Santa Sandra Alum, Francis Barnabas Gonahasa na Kenneth Esiangu Eitunganane.