Bajeti ya serikali inatarajiwa kupitishwa na wabunge mjini Dodoma leo, wabunge wamendelea kuunga mkono juhudi za Rais John Mgufuli kwa kulinda rasilimali za nchi huku wakisisitiza kuwa vita ya madini ni vita ambayo kila mtu bila kujali itikadi za kisiasa anaiunga mkono.

Akichangia mjadala wa Taarifa ya hali ya uchumi 2016 na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliyowasilishwa bungeni Juni 8 mwaka juu, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, alimpongeza Rais Dk Magufuli na kuwa ni wakati wa kumuunga mkono kutokana na kazi kubwa aliyofanya kwa kusimamia mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi ‘makinikia’ na kusisitiza haja ya kuunga mkono pia juhudi za marais waliopita.

Nape alisema wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, kuna mambo aliyafanya katika kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa na kwamba kuna mambo alifanya hata kama kuna mapungufu.

Awamu zingine ni Awamu ya Pili ya Ali Hassani Mwinyi, ya tatu, Benjamin Mkapa na wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. “Hakuna haja ya kupuuza juhudi za watangulizi wake kwa sababu nao walitoa mchango hata kama itaonekana kulikuwa na mapungufu, lakini kwa nafasi zao walitimiza wajibu.

Tunatakiwa tutambue na kuheshimu michango yao badala ya kubaki tunawanyooshea vidole kama vile hawakufanya lolote,” alisema na kusisitiza kuwa Rais Magufuli ameifikisha nchi katika hatua kubwa zaidi. Aliongeza kuwa, “Kelele zisiturudishe nyuma lazima tusonge mbele kwa sababu vita hii ni takatifu, lakini tusipuuze katika kelele nyingi kwani kunaweza kukawa na ushauri mzuri ndani yake.

Hii vita ni ya kwetu wote, sasa tusitoboane macho tusitupiane vijembe visivyokuwa na sababu, ni wakati wa kuileta nchi yetu pamoja twende tukapigane vita tuishinde.” Kuhusu uchumi wa gesi na mafuta, Nape alirejea upotoshwaji wa taarifa na kuwa zilijaa chumvi nyingi badala ya ukweli kwamba faida ya gesi ingeweza kuonekana baada ya miaka 20 au 30, jambo ambalo lilisababisha vurugu. Alitumia fursa hiyo kuihoji serikali utekelezaji wa mradi wa mitambo ya kuchakata gesi, ambao alisema kukamilika kungeleta manufaa ya haraka kwa wananchi wa eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *