Wabunge nchini Korea Kusini wamepiga kura kumuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo Park Geun-hye kutokana na matumizi mabaya ya madaraka.

Maelfu ya waandamanaji walikuwa wamekusanyika nje ya majengo ya bunge mjini Seoul wakitaka Park aondolewe madarakani.

Hatua hiyo itamlazimisha bi Park kung’atuka kwa muda huku Mahakama ya Kikatiba ikiamua iwapo ataondolewa kabisa kwenye wadhifa huo wa urais.

Suala kuu limekuwa ni uhusiano kati ya Bi Park na msiri wake mkuu Choi Soon-sil, ambaye anadaiwa kutumia uhusiano huo kujizolea ushawishi nchini humo.

Viongozi wa mashtaka wamesema Bi Park alikuwa na “mchango mkubwa” katika visa kadha vya ufisadi, tuhuma ambazo amezikanusha.

Bunge la Korea Kusini lilianzisha hoja hiyo jana ambapo iilihitaji kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya wabunge ndipo kupitishwa.

Bunge linatawaliwa na vyama vya upinzani na wabunge huru ambao wanataka aondolewe madarakani, lakini walihitaji wabunge 28 zaidi kutoka kwa chama cha Saenuri, chake Bi Park, ndipo wafikishe idadi ya kura inayohitajika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *