Waathirika wa tetemeko la ardhi katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wameiomba serikali iwaongezee mahema ili waepuke adha ya kunyeshewa na mvua.

Wamesema kutokana na mvua kubwa yenye upepo mkali iliyonyesha usiku wa kuamkia jana, imesababisha kero na usumbufu mkubwa kwa waathirika hao.

Mkazi wa mtaa wa Car Wash katika kata ya Hamugembe, Adventina William amesema, kutokana na mvua iliyonyesha jana usiku wamepata usumbufu mkubwa usiku mzima hali iliyowafanya washindwe kulala na kusimama usiku kucha.

Mkazi wa mtaa wa Nyangoye, kata ya Hamugembe, Mariastella John alisema hadi sasa hakuna msaada wowote wa maana aliopokea kutoka serikalini zaidi ya kilo moja ya sukari, mchele, maharage na hema moja.

“Sisi tumepewa hema moja na tunaishi humu familia ya watu 12 wakiwamo watoto, kwa kweli hali zetu ni mbaya serikali ituangalie zaidi,” alisema.

Joanita John ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Hamkisheni, alisema mvua iliyonyesha usiku kucha imesababisha yeye na watoto wake watatu kulala nje na baridi kali.

“Mpaka sasa sijapata msaada wowote kutoka serikalini nilikuwa nalalia mito ya makochi na wanangu, ila jana nililalia mifuko ya sandarusi baada ya maji kuingia ndani,” alieleza.

Mtendaji wa Kata ya Hamugembe, Sudi Zuberi alisema kata yake imeathirika na tetemeko la ardhi kuliko kata zote kwani jumla ya nyumba 606, zimeanguka.

“Kata yangu imeathirika na tetemeko na misaada tunayopewa tuwapatie waathirika kwa kweli bado haitoshi. Juzi nilipewa mahema 150 nigawe mahema mawili kwa kila kaya, lakini kaya zilizopata mahema ni 75 tu na bado kuna kaya 55 hazijawahi pata kabisa msaada wowote,” alisema mtendaji huyo.

Amesema, wanachopewa na Kamati ya Maafa ya Mkoa ndicho wanachofikisha kwa wananchi kama walivyopokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *