Benki ya NBC imetangaza kuvipiga mnada shule na vyuo vya Eckernforde vya mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa tangazo la benki hiyo lililotolewa katikati ya wiki hii na Kampuni ya udalali ya Bani Investment Limited, Debt Collectors/Auctioneers na kuchapishwa katika magazeti mawili ya kila siku (si MTANZANIA Jumapili), limetanabaisha kuwa mnada wa chuo hicho pamoja na shule zake utafanywa Machi 11.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Bani, Lita Colyvas, alisema taratibu za kutekeleza mnada wa vyuo vya Eckernforde umefuatwa kisheria.
Alivitaja vyuo hivyo kuwa ni kile kilichojengwa kwenye kiwanja namba 53/2 na kiwanja namba 54/2, CT namba 2532, LO namba 62988, kitalu 111 chenye ukubwa wa mita za mraba 921 ambacho kipo eneo la Central Tanga.
Chuo kingine ni cha ualimu pamoja na sekondari ambacho kina ukubwa wa ekari 3,426 kwenye kiwanja namba 12, CT namba 18517, LO namba 170760 katika eneo la Kange Tanga.
Amesema kuwa vyuo hivyo vinatambulika kwa jina la Eckernforde Education Company Limited.