Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imewaachia huru viongozi wa chama cha madaktari waliokuwa wamefungwa jela mwezi mmoja kutokana na kuendeleza migomo.
Viongozi hao saba walifungwa jela siku ya Jumatatu baada ya kupatikana na hatia ya kutofuata uamuzi wa mahakama wa kumaliza mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa miezi miwili unusu sasa.
Viongozi hao wametakiwa kuhakikisha suluhu ya mgomo huo inapatikana katika kipindi cha siku saba.
Mazungumzo ya kutafuta suluhu yataongozwa na Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNHCR).
Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara na kuboresha mazingira ya utendaji kazi hospitalini
Wanataka pia serikali iwekeze zaidi katika dawa, vifaa na mitambo hospitalini pamoja na kutoa pesa zaidi za kufadhili utafiti wa kimatibabu.