Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe (62) na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na rushwa ya Sh bilioni nane.
Vigogo wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa zamani wa Uhandisi wa TPA, Bakari Kilo (59) na aliyekuwa Meneja wa Mazingira wa TPA, Theophil Kimaro (54) pamoja na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Wakili Kishenyi amedai katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2009 na 2012, Mgawe, Kilo na Kimaro kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ya Dola za Marekani milioni nne ikiwa ni zaidi ya Sh bilioni nane.
Inadaiwa waliomba rushwa hiyo kutoka kwa Shapriya ili kumuwezesha ashinde zabuni iliyokuwa ikishindaniwa yenye namba AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la TPA katika RAS ya Mjimwema.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009 akiwa kama Mkurugenzi wa DB Shapriya alitoa rushwa ya Dola za Marekani milioni nne kwa vigogo hao, kwa ajili ya kuiwezesha kampuni yake ishinde zabuni.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa walikana kuhusika na kutenda makosa hayo.
Wakili Kishenyi alisema upelelezi wa kesi bado unaendelea, pia hawana pingamizi la dhamana endapo washtakiwa watatimiza masharti ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.
Washtakiwa waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili waaminifu watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni 500 kwa kila mmoja.