Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema inatarajia kutayarisha mwongozo wa kupiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani ili kudhibiti maradhi ya kuambukiza.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu uvutaji wa sigara katika sehemu za mkusanyiko na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Waziri huyo amesema kuwa tayari Wizara ya Afya imewasilisha muswada wa kulinda afya ya jamii ambao moja ya kazi yake kubwa ni kupambana na matumizi ya sigara katika jamii na sehemu za mkusanyiko.
Ameongeza kwa kusema kuwa utafiti uliofanywa kuhusu maradhi yasiyoambukiza unaonesha kwamba upo kwa asilimia 38 ambayo yanahusishwa na uvutaji wa sigara. Kombo alisema mwongozo huo ukikamilika utaletwa mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe kutoa maoni yao kabla ya kufanya kazi na kuwa sheria inayotakiwa kutekelezwa na kusimamiwa.
Pia amesema yapo matumizi mabaya ya uvutaji wa sigara hadharani ikiwemo sehemu za mikusanyiko ya watu kama hospitalini na sehemu za kusubiri usafiri wa abiria na kusababisha madhara makubwa ambayo hayaonekani kwa mara moja.