Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM umelitaka Baraza la Vijana la Chadema BAVICHA kuacha kuingilia majukumu ya vyombo vya dola badala yake waviache vifanye kazi zake za kiuchunguzi ili vitoke na majibu sahihi kuhusiana na baadhi ya matukio ya watu kutekwa na kuuawa.

Akizungumza hii leo Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alimtaka Mweneykiti wa BAVICHA, Patrick Ole Sosopi kuacha kuviingilia vyombo vya dola katika ufanyaji kazi wake kwani masuala yote ya kiuchunguzi, kintelejinsia na kiutawala ni siri na hayawezi kuchukuliwa kisiasa kama anavyofikiria.

Amesema Bavicha wanapaswa kutambua kuwa serikali yenye vyombo vya dola ni tofauti na serikali ya wanafunzi hivyo wasiichukulie kiwepesi hadhi ya Rais aliyepo madarakani kisheria na kikatiba maana Rais wa Nchi siyo sawa na rais wa chama cha mpira.

“Bavicha kwanini wajawe na hofu ya kutoviamini vyombo vya dola. Masuala ya kintelejinsia ,uchunguzi na upelelezi ni nyeti .Yanaweza kumuhusisha mtu moja moja, kikundi au mtandao hivyo si jambo la kuhemkwa na kukurupuka.

” Namshangaaa sana Sosopi kwa kuyalinganisha masuala ya Tanzania na Uganda huku akionyesha kuwa na ufahamu mfupi kwani Joseph Kony na kikosi chake cha uasi wanaisumbua serikali ya Uganda kwa miaka mingi na hadi sasa hajakamatwa wala kiongozi mwenye dhamana kujiuzulu,” alisema Shaka.

Aliongeza kuwa kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na IGP siyo jawabu la kumaliza matatizo na kumtaka kuwa na adabu na heshima mbele ya Rais Magufuli na aache kumuamuru Rais kutengua nafasi za viongozi hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *