Utafiti mpya uliofanywa na kuchapishwa kwenye jarida la BMC Public Health Journal umeonyesha kuwa matumizi ya dawa za kukabiliana na bakteria ni mabaya barani Afrika.
Utafiti huo unaonyesha kuwa madaktari wa Afrika huwaandikia dozi kubwa za dawa wagonjwa wao kuliko inavyoshauriwa na muongozo wa tiba wa World Health Organization (WHO).
Tatizo hilo hupelekea matumizi mabaya ya dawa au matumizi makubwa ya dawa na kusababisha usugu wa maradhi kwa watumiaji.
Watafiti kutoka chuo kikuu cha London na Health Policy Consult cha Ghana walipitia tafiti nyingine za utolewaji wa dawa kwenye nchi 11 za Afrika na kukuta kila mara mgonjwa anapokutana na daktari huandikiwa wastani wa dawa tatu huku WHO ikishauri zisizidi dawa mbili kila mgonjwa anapokwenda hospitali.
Watafiti hao pia wamegundua kuwa mara nyingi kwenye taasisi za afya zisizo za umma wagonjwa huandikiwa dawa nyingi kwaajili ya taasisi kuingiza fedha zaidi.