Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Snura amewataka wachezaji wa Simba kuelekeza nguvu zao kwenye ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya kutolewa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.
Snura ambaye ni shabiki mkubwa wa timu hiyo, ameeleza hisia zake kwa kikosi hicho baada ya kushindwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba iliondolewa kwenye michuano hiyo na timu ya Al Masry ya Misri baada ya kutoka sare ya 2-2 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushindwa kuifunga timu hiyo katika mchezo wa ugenini.
Snura aliwapa moyo wachezaji hao huku akiamini ubingwa ndio utawapunguzia machungu baada ya kutolewa kwenye michuano hiyo.
Pia Snura ameongeza kwa kusema kuwa kutokana na kiwango cha wachezaji wa Simba ni dhahiri ubingwa kwao hauzuiliki huku akiwataka kuongeza umakini kwa kuwa wapinzani wao nao wapo kwenye mbio hizo.