Kesi inayomkabili muigizaji wa Bongo Movie, Wema Sepetu leo imehairishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kutokana na upelelezi kutokamilika.
Muigizaji huyo anakabiliwa na kosa la kukutwa na bangi katika upekuzi uliofanywa na polisi nyumbani kwake Februari 4, mwaka huu maeneo ya Ununio jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilipelekwa leo kwa ajili ya kutajwa ambapo Wakili wa Serikali Nasoro Katuga amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo Hakimu Mkazi Thomas Simba ameahirisha shauri hilo hadi Machi 15.
Wema alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 9, mwaka huu ambapo aliachiwa baada ya kupata dhamana ya Sh milioni tano.
Muigizaji huyo ni miongoni mwa wasanii waliotajwa kwenye orodha ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wanaojihusisha na masuala ya madawa ya kulevya ambao walitakiwa kuripoti kituo cha Polisi mapema mwezi huu.