Baraza la Usalama la umoja wa mataifa (UN) limetoa wito kwa wagombea wakuu na wafuasi wao nchini Gabon kujizuia kufanya fujo na badala yake kutatua mzozo wa sasa kupitia njia za kisheria.

Maafisa wa usalama wamewakamata watu zaidi ya elfu moja baada ya siku ya pili ya maandamano ya wafuasi wa upinzani baada ya matokeo ya uchaguzi nchin humo.

Upande wa upinzani unadai Rais Ali Bongo aliiba kura wakati wa uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Rais Bongo amesisitiza kwamba alishinda kwa njia halali na kuutaja ushindi wake kuwa ushindi wa watu wa Gabon huku akisema kuna kundi dogo la watu wachache waliotaka kutwaa madaraka na ambao wameshindwa.

Matokeo ya uchaguzi yalitangazwa Jumatano alasiri na kumpatia Rais Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura akifuatwa na Jean Ping aliyepata 48.2 % ya kura kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.

Kwa upande wa Bw Ping amesema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na hakuna ajuaye hasa nani alishinda kwenye uchaguzi huo.

Bw Ping amesema takwimu kutoka ngome za rais huyo zinaonyesha asilimia 99 ya wapiga kura walijitokeza huku akiomba takwimu za wapiga kura kutoka kila kituo zitolewe wazi.

Rais Bongo aliingia madarakani mwaka wa 2009 baada ya kifo cha baba yake aliyekuwa ameongoza taifa hilo tangu 1967 mpaka alipofariki mwaka 2009.

Ping kabla ajaingia kwenye siasa aliwahi kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *