Umoja wa Afrika (AU) umelaani matamshi ya dharau na kuishushia hadhi Afrika aliyotoa Rais Donald Trump alipokutana na wabunge kwenye ofisi yake ya mviringo ikulu.
Vyombo vya habari vya Marekani yakiwemo mashirika makubwa kama CNN na Washington Post yalinukuu vyanzo vya uhakika kwamba Trump aliyaita mataifa ya Haiti, El Salvador na Afrika kuwa “mataifa machafu”.
Katika kikao hicho Alhamisi iliyopita Trump inadaiwa alihoji: “Kwa nini tunawaruhusu watu hawa kutoka “nchi chafu” kuingia nchini?”
Botswana imekuwa nchi ya kwanza Afrika kumshutumu Trump kwa kuyaita mataifa ya Afrika kuwa “machafu” na ikasema tamko la rais huyo ni la kukosa kuwajibika.
Pia imechukua hatua ya kumwita balozi wa Marekani aliyeko Botswana aweze kufafanua iwapo Marekani inachukulia taifa hilo la kusini mwa Afrika kama “taifa chafu” na taifa la mabwege.
Botswana imeitaka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika Sadc pamoja na Umoja wa Afrika kushutumu tamko hilo la Trump.