Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard imeihakikishia Serikali kuwa meli mpya mbili za mizigo zinazoendelea kujengwa katika Bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya zitakuwa zimekamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Salehe Songoro amesema ifikapo Oktoba 30, mwaka huu kampuni hiyo itaziingiza meli hizo mbili za mizigo ndani ya ziwa Nyasa tayari kwa safari za majaribio.

Ametoa uhakika huo juzi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kufanya ziara ya kushitukiza bandarini Itungi akilenga kufuatilia ujenzi huo wa meli mpya.

Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa ujenzi wa meli mbili za mizigo umefikia zaidi ya asilimia 80, hivyo kazi zilizosalia ni za umaliziaji ikiwemo upakaji rangi na tayari meli hizo zimepewa majina ya Mv Ruvuma na Mv Njombe.

Amesema meli ya abiria ambayo ujenzi wake utakamilika Februari mwakani itapewa jina la Mv Mbeya II kwa kuwa jina la Mv Mbeya liliwahi kutumika miaka ya nyuma katika meli iliyozama ndani ya Ziwa Nyasa miaka mingi iliyopita.

Akitoa tathmini yake baada ya ziara hiyo, Makalla alisema ameridhishwa na hatua za ujenzi huo na kuwa ana imani kuwa ahadi ya kuziingiza ziwani meli mbili za mizigo mwishoni mwa mwezi huu itatimizwa.

Amesema tayari wadau mbalimbali wa kibiashara wameanza kuonesha nia ya kutumia usafiri huo mara tu utakapoanza kutoa huduma.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *