Kikundi cha waasi wa Alliance of Democratic Forces (ADF) kimetajwa na ripoti maalum ya uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa kuwa kilihusika na mauaji ya askari wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UN, ushahidi uliopatikana unaonyesha ADF ndio walifanya shambulizi hilo la kushtukiza na kusababisha vifo vya askari hao waliokuwa wakilinda amani nchini huko Januari 5, mwaka 2018.

Kufuatia mauaji hayo Katibu Mkuu wa UN aliagiza kufanyika uchunguzi maalumu ulioongozwa na Katibu Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Taasisi za Sheria na Usalama, Dmitry Titov.

Uchunguzi huo ulijikita katika mfululizo wa matukio ya mashambulizi dhidi ya walinda usalama wa UN katika eneo la Beni, jimbo la Kaskazini Kivu, DRC.

Vilevile timu hiyo maalumu ilipewa jukumu la kuchunguza tukio la shambulizi la Desemba 7, mwaka jana ambapo walinda usalama 15 wa Tanzania waliuawa katika kituo chao Semuliki, huku 43 wakijeruhiwa na mmoja mpaka sasa hajulikani alipo.

Uchunguzi huo pia umehusisha mashambulizi mawili ya awali dhidi ya walinda usalama wa Tanzania yaliyotokea karibu na Mamundioma Septemba 16 na Oktoba 7, 2017.

Timu hiyo maalumu ya uchunguzi ambayo iliwaleta pamoja wataalamu wa jeshi na usalama, wanasiasa na maofisa wa mipango ya vita na maofisa wa juu wa Tanzania kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ililenga kutambua mazingira yaliyopelekea mashambulizi hayo, kutathmini hatua za MONUSCO na kubainisha hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ili kuzuia mashambulizi yasitokee siku za usoni.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *