Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Kenya imetangaza kwamba uchaguzi mpya wa urais nchini humo utafanyika tarehe 17 Oktoba.
Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati amesema uchaguzi huo utashirikisha wagombea wawili pekee wa urais, Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.
Waliopinga matokeo ya uchaguzi kortini, Bw Raila Odinga na mgombea mwenza wake Stephen Kalonzo Musyoka na mshtakiwa wa tatu Rais Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza wake William Samoei Ruto, watakuwa ndio wagombea pekee.
Katika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Mahakama ya Juu iliiwekea lawama Tume ya Uchaguzi.
Majaji wa tume hiyo hawakuandaa uchanguzi huo kwa viwango vilivyowekwa kwenye katiba na sheria za uchaguzi, na kwamba kulitokea kasoro nyingi sana katika mchakato wa kupeperusha matokeo.
Chebukati amesema tume hiyo inafanyia utathmini mifumo na taratibu zake kwa ajili ya uchaguzi huo mpya.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na IEBC kuhusu uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.