Taasisi inayotoa tuzo za Utawala bora ya MO Ibrahim imetangaza kukosa mshindi kwa mwaka 2016, inayotolewa kwa viongozi wa Afrika waliostaafu.
Hayo yamesemwa kwenye mkutano wa kamati uhuru ya tuzo hiyo, chini ya mweyekiti wa Dr Salim Ahmed Salim pamoja na mkutano wa bodi ya taasisisi hiyo iliofanyika mwishoni mwa wiki lililopita.
Akizungumzia juu ya uamuzi wa kamati ya tuzo hiyo ya Mo Ibrahim, Dr Salim alisema ” kama ninavyosisitiza kila mwaka , paliwekwa kipimo cha hali ya juu, wakati tukizindua tuzo hii 2006.
Dr Salim akaongeza kusema kwamba baada ya zingatio makini, kamati hiyo imeamua kutomzawadia yeyote tuzo hiyo kwa mwaka 2016.
Wagombea wote wa tuzo ya Ibrahim ni ama Viongozi wa taifa au Serikali waliondoka madarakani katika kipindi cha miaka mitatu iliopita na ambao walikuwa wamechaguliwa kidemokrasi na kutumikia vipindi vyao kwa mujibu wa katiba.
Tangu ilipoanzishwa 2006, tuzo ya Mo Ibrahim imeshatolewa mara nne. Washindi waliopita ambao wote walikuwa marais wa nchi zao ni, Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014), Pedro Pires wa visiwa vya Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2008). Rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela alitunukiwa tuzo ya heshima 2007.