Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu na wenzake wamelikomalia vilivyo sakata la kughushi vyeti vya kielimu linalomkabili mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu amesema uamuzi huo wa kulifikisha mahakamani suala hilo la kufoji vyeti umetokana na maazimio ya baraza la uongozi la chama hicho, lengo likiwa ni kulinda utawala wa sheria na uwajibikaji nchini.
Tofauti na matarajio ya baadhi ya watu kwenye ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wote wa umma iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ijumaa kutowagusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wabunge na madiwani.
Katika kufanikisha nia hiyo ya TLS, Lissu aliyekuwa na viongozi wengine wa chama hicho wakiwamo Makamu Rais, Godwin Ngwilimi na Wakili Stephen Kuwayawaya, alisema miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na TLS kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya mkuu huyo wa mkoa.
Aliongeza kuwa mkuu huyo wa mkoa, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai likiwamo hilo la kutumia vyeti feki na kwamba, kazi ya kumshtaki haitachukua miezi bali ni wiki mbili au tatu.