Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amekibeza Chama cha ACT Wazalendo kwa kudai kuwa kuteuliwa kwa viongozi wake katika Serikali ya Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ ni kama kupewa zawadi kwa kazi yao waliyoifanya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Akizungumza nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, jana, Lissu alisema ACT ilianzishwa ili kuua upinzani hivyo baada ya kuifanya kazi yao, sasa wanapewa kama zawadi kwa viongozi wake kuteuliwa serikalini.
Akijibu swali kama yeye akiteuliwa atakubali au la, Lissu alisema kwanza hawezi kuteuliwa, lakini pia hata akiteuliwa, hatakubali.
“Kwanza haitatokea rais aniteue kwenye nafasi yoyote na kama akiniteua basi nitamwambia mheshimiwa, mimi napinga mfumo uliokuweka madarakani, nataka katiba mpya, nataka tutengeneze mfumo mpya wenye misingi sawa, ya kuiongoza nchi,” alisema Lissu.
Rais Magufuli alimteua na kumuapisha aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, ikiwa ni wiki chache tangu alipofanya uteuzi wa mwanachama mwingine wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.