Afya ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji, inazidi kuimarika na sasa anaweza kufanya mambo mengi mwenyewe ikiwamo kwenda kuoga na kutembea kwa kutumia magongo.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), alipelekwa Ubelgiji Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana.
Mbunge huyo aliumia vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana, tano kati ya hizo zikimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Vinceti Mghwai, ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema jana kuwa Lissu ameanza kutembea mwenyewe kwa kutumia magongo na kujipatia huduma mbalimbali ikiwemo kwenda kuoga bila msaada wa mtu mwingine.
Mghwai alisema Lissu anapata muda mwingi wa kupumzika na huenda hiyo ndiyo ikawa sababu kubwa ya yeye kuendelea kupona haraka kutokana na kupatiwa matibabu na bila usumbufu wowote.
Alisema Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa Hospitali ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu waliokuwa wakienda kumjulia hali.