Rais wa Marekani Donald Trump amesema angependa kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ili wazungumzo kuhusu mpango wa kinyuklia.

Tamko la Bw Trump limetokea huku wasiwasi ukiendelea kuongezeka kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Kwa upande wa Ikulu ya White House ilitoa taarifa kufafanua matamshi ya Trump na kusema Korea Kaskazini ingehitaji kutimisha masharti mengi kabla ya mkutano kati ya viongozi hao wawili kufanyika.

Msemaji wa ikulu hiyo Sean Spicer amesema Washington inataka kuona tabia ya uchokozi ya Korea Kaskazini ikikoma mara moja.

Siku ya Jumamosi Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kurusha kombora la masafa marefu ambalo lilifeli, mara ya pili kwa jaribio kama hilo kutekelezwa na Pyongyang katika kipindi cha wiki mbili.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka siku za karibuni, huku Korea Kaskazini na Kusini zikifanya mzoezi ya kijeshi.

Marekani imetuma meli za kivita na nyambizi eneo hilo na pia imeweka mtambo wa kutungua makombora ya adui Korea Kusini, mtambo ambao maafisa wanasema umeanza kufanya kazi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *