Rais wa Marekani Donald Trump alifichua taarifa zinazofaa kuwa siri kuu kuhusu kundi linalojiita Islamic State (IS) kwa waziri wa mambo ya nje wa urusi.
Taarifa hizo, zilihusu kutumiwa kwa laptopu kwenye ndege, na zilitoka kwa mshirika wa Marekani ambaye hakuwa ametoa idhini kwa habari hizo kukabidhiwa Urusi.
Mshauri mkuu wa usalama wa taifa wa Marekani HR McMaster amepuuzilia mbali madai hayo kwenye vyombo vya habari na kusema ni ya uongo.
Tuhuma kwamba huenda maafisa wa kampeni wa Bw Trump waliwasiliana na maafisa wa Urusi zimegubika utawala wa rais huyo, na kufikia sasa uchunguzi unaendelea.
Wakati wa kampeni, Bw Trump alimkosoa sana mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton, kwa jinsi alivyoshughulikia taarifa ambazo zinafaa kuwa siri kuu.
Katika mazungumzo yake na Lavrov pamoja na balozi wa Urusi nchini Marekani katika afisi yake White House, trump alifichua maelezo ambayo huenda yakapelekea kutambuliwa kwa mdokezi aliyetoa habari hizo, maafisa waliambia Washington Post na New York Times.
Walizungumzia njama ya IS. Rais huyo inadaiwa alianza kuzungumzia mambo ambayo alikuwa hajapangiwa kuyazungumza, na kufichua maelezo zaidi kuhusu njama hiyo.
Njama hiyo inadaiwa kujumuisha kutumiwa kwa laptop kwenye ndege. Mazungumzo ya trump yaligusia ni jiji gani kulikuwa kumegunduliwa tishio.
Habari hizo za kijasusi zilitoka kwa mshirika wa Marekani na zilichukuliwa kuwa za usiri mkubwa kiasi kwamba hazikufaa kufahamishwa washirika wengine wa Marekani, magazeti hayo yameripoti.
Wengine waliokuwepo katika mkutano huo waligundua kosa hilo la Bw Trump na wakachukua hatua kujaribu kuzima moto huo kwa kuwafahamisha maafisa wa CIA na maafisa wa Shirika la Usalama wa taifa (NSA), gazeti la Washington Post linasema.