Kampuni  ya Reli Tanzania (TRL) imekanusha kuhusika na vichwa 11 vya treni vilivyoshushwa na kutelekezwa katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, vichwa hivyo vilivyoshushwa na meli ya Mesina Line tangu wiki iliyopita, na kwamba ni mali ya TRL.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Masanja Kadogosa jana alisema TRL haihusiki kwa namna yoyote na vichwa hivyo kwa kuwa hakuna taarifa zozote zinahusu uagizwaji wake.

Amesema pia kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi, kampuni hiyo inapofanya manunuzi yoyote lazima kuwepo na mkataba wa makubaliano na kampuni husika inayouza bidhaa, lakini haina mkataba wowote unaohusu ununuzi wa vichwa hivyo.

Alieleza kuwa taratibu za manunuzi zinafahamika kwani endapo kampuni hiyo ingeagiza vichwa hivyo ingetakiwa kupeleka mtu wake kwa ajili ya ukaguzi wakati vinatengenezwa na mara baada ya kutengenezwa kabla ya kupakiwa kwenye meli. “Lakini hiyo kitu hakuna, hatukuwa na watu wetu kwa kuwa si mali yetu,” alieleza.

Pamoja na hayo, alisema ili mzigo wowote umfikie mhusika lazima kuwepo na nyaraka ya kutolea mzigo bandarini ambayo pia huwa na makubaliano mengine baina ya mnunuzi na muuzaji ambayo katika sakata hilo, TRL wamesisitiza hawana nyaraka hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *