Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya udalali ya Yono Action Mart ilivamia ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kutaka kufunga ofisi hizo kutokana na kudaiwa deni la Sh bilioni 1.6.

Maofisa hao wa TRA wakiongozana na madalali wa Yono walitinga ofisi hizo za TFF zilizopo Karume, Ilala na kuanza kufunga mageti na baadhi ya magari yaliyokuwa yameegeshwa kwenye ofisi za shirikisho hilo huku wahusika wa magari hayo wakitakiwa kutoka kwa kitambulisho ili kujua magari yanayomilikiwa na TFF.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliwaomba maofisa hao wa TRA kuzungumza na baada ya mazungumzo ya muda mrefu kidogo TRA na Yono wakaondoka kwa makubaliano kuwa TFF watamalizana nao leo hadi kufikia saa nne asubuhi.

Meneja Operesheni wa Yono, Kasimir Mwandema alisema kuwa wanachofanya wao ni kutekeleza agizo la TRA kwa kukamata mali za TFF ili kufidia deni la Sh bilioni 1.6.

Amesema TRA imekuwa ikiwadai Sh bilioni 1.118 ambayo ni kodi mchanganyiko kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, kodi hizo VAT, Kodi ya Mapato, SBL na kwamba hapo nyuma walikamata akaunti zao kwa sababu deni lilikuwa ni Sh bilioni 1.6 na wakapunguza sehemu ya deni lakini halijaisha ndio sababu wanataka kukamata tena mali za TFF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *