Wizara ya Maji na Umwagiliaji imebainisha kuwa iko kwenye mchakato wa kuondoa tozo ya huduma kwenye mita za maji kama ilivyofanyika kwenye huduma za umeme.

Tayari wizara hiyo imeanza kufanya majaribio kwa kuondoa tozo hiyo kwa mita za maji mkoani Iringa, ambapo pia mita za maji nchi nzima zitawekwa mfumo wa kulipia kadiri mteja anavyotumia kama ilivyo katika umeme inayotumia mfumo wa LUKU ili kuwaondolea usumbufu wateja wa maji.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge ameyasema hayo Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema).

Gekul alitaka kujua wizara hiyo ina mpango gani wa kuwaondolea mzigo wa tozo wananchi ya huduma kama ambavyo Wizara ya Nishati na Madini ilivyoondoa tozo hiyo kwenye mita za LUKU za umeme.

Akijibu, Lwenge alisema tayari mchakato huo umeanza mkoani Iringa ambapo sasa wananchi wa mkoa huo wanalipia maji wanayotumia bila tozo hiyo ya huduma, lakini pia mita zao ni za LUKU hivyo hakuna ulazima kwa watendaji kusoma mita hizo.

Awali, katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema), alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kupunguza bei ya huduma ya maji ili wananchi waweze, kumudu huduma hiyo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alisema utaratibu wa kuongeza bei ya maji ni wa kawaida na upo kisheria.

Alikiri kuwa mkoani Shinyanga kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (SHUWASA) imepandisha bei ya maji kuanzia Septemba mwaka 2015, baada ya kupata kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA).

Source: Habari Leo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *