Timu iliyondwa na waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye leo inatarajiwa kutoa ripoti kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha Habari cha Clouds Media akiwa na askari wenye silaha.

Waziri Nape jana aliunda timu ya watu watano kwa ajili ya kuchunguza sakata lililofanywa na mkuu wa mkoa huyo kwa kuvamia ofisi za Media hiyo.

Nape amesema kama serikali, kilichotokea ni kitendo ambacho kimewashtua wengi na hata dunia kwa ujumla kwa kuwa hata katika historia haijawahi kutokea suala kama hilo.

Waziri huyo ameunda timu hiyo kwa ajili ya kufanya kazi kwa saa 24 ili kujua na upande wa pili ambao ni wa Makonda unazungumziaje suala hilo na baadaye watamkabidhi ripoti hiyo.

Timu hiyo inaundwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Abbas Hassan, ni Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi, Mhariri Mwandamizi kutoka Kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamhuri na Mhariri wa Wapo Radio, Neng’ida Johannes.

Waziri Nape amesema serikali imesikitishwa na jambo hilo, lakini lazima kutenda haki kwa kumsikiliza pia mkuu wa mkoa na watu wake ili kujiridhisha halafu ndipo hatua nyingine zitakapoweza kuchukuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *