Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye amesema kuwa mfumo wa kuingia uwanja wa Taifa kwa tiketi za Elektroniki utaanza kutumika rasmi oktoba 1 mwaka huu kwenye mechi ya Simba na Yanga.
Nnauye amesema kabla ya mfumo huo wa kieletroniki kuanza kutumika rasmi katika mchezo wa Simba na Yanga Oktoba 1 utafanyiwa majaribio mara mbili au tatu ili mashabiki kuelewa zaidi.
Aidha Waziri Nape pia amebainisha kuwa hakuna gharama za ziada ambayo Serikali imeingia katika ufungaji wa mfumo huo wa kieletroniki uwanjani hapo kwani hilo lilikuwa ndani ya mkataba wa wajenzi wa uwanja huo kampuni ya BCG.
Kwa mujibu wa Meneja Mradi na mshauri wa mifumo wa Selcom Gallus Runyeta mfumo huo unaweza kupitisha watu 100,002 kwa saa tatu hivyo kuondoa uwezekano wa kuwepo msongamano wakati wa kuingia uwanjani.
Mfumo huo wa tiketi za Elektroniki umefungwa na Selcom ambao ndiyo wamepewa zabuni ya kufunga mfumo huo.