Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka amesema amekabidhiwa tuzo nchini Marekani, lakini amekataa kupokea fedha zinazoambatana na tuzo hiyo ambazo ni Dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh milioni 200) kutokana na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo iliwahi kumtia matatani.
Profesa Tibaijuka alisema tuzo hiyo ni ya Maendeleo Endelevu ya Mwana wa Mfalme Khalifa bin Salman Al Khalifa wa Bahrain ambazo zilitolewa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani usiku wa Septemba 23, mwaka huu.
Amesema ameshinda tuzo hiyo ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuhamasisha maendeleo duniani na sherehe za utoaji wa tuzo hizo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali duniani wakiwemo mabalozi na mawaziri.
Tuzo hizo hutolewa kila baada ya miaka miwili ambapo washiriki wakuu huwa ni wale waliowahi kufanya kazi Umoja wa Mataifa.
Profesa Tibaijuka aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat).