Shirikisho la soka Tanzania (TFF), limetoa rambirambi ya Sh 500,000 kwa walengwa walipoteza watoto katika ajali ya gari iliyoua zaidi ya watu 36, wakiwamo wanafunzi 33.

Rambirambi hiyo ya TFF inakwenda sambamba na salamu za rambirambi zilizotolewa na Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi aliyeungana na viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuomboleza msiba huo.

Rais Malinzi amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo hivyo kwani imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia taifa katika tasnia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu kama wachezaji, makocha, viongozi hapo baadaye.

Salamu za Rais Malinzi zimekwenda kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, akisema: “Huu ni wakati mgumu kwa Wana – Arusha, wazazi na walezi hawana budi kuwa na subira kwa sasa.”

Amesema kwamba kwa wanafamilia wote wa mpira wa miguu, “Tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema. Pia wale waliopata majeruhi tunaomba wapone haraka katika ajali hiyo mbaya. Ee Mwenyezi Mungu zipumzishe Roho za Marehemu hao, Mahala pema peponi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *