Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kamati yake ya maudhui inafuatilia mahojiano ya mwanamuziki huyo aliyoyafanya katika kituo hicho.
Ofisa Mkuu Idara ya Utangazaji ya mamlaka hiyo, Andrew Kisaka amesema wamechukua uamuzi huo kwa kuwa mahojiano hayo yamefanyika katika kituo wanachokisimamia.
Katika mahojiano hayo, Diamond alimjibu Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza kutokana na Serikali kuzifungia nyimbo 15 mwezi uliopita, zikiwemo mbili za mwanamuziki huyo.
Kisaka amesema kuwa kiutaratibu wao wanaangalia zaidi chombo ambacho wamekipa leseni na kwamba, masuala mengine yatashughulikiwa na mamlaka nyingine.
Amesema suala hilo kwa sasa linafanyiwa kazi na kamati ya maudhui na kuahidi kulitolea ufafanuzi siku za hivi karibuni akiwataka wananchi kuwa na subira.